WIZARA YA UCHUKUZI YAENDELEA NA MAANDALIZI YA KIKAO CHA 19 CHA TATHMINI YA UTENDAJI WA SEKTA YA UCHUKUZI
Wizara ya Uchukuzi imeendelea na maandalizi ya Kikao cha 19 cha Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (Joint Transport Sector Review Meeting – JTSR), kupitia kikao cha pili cha Kamati ya Maandalizi kilichofanyika tarehe 30 Septemba 2026 katika Ofisi za Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mkonze, Dodoma.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Bi. Devota Gabriel, amewataka wajumbe wa Kamati kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ushirikiano na kuzingatia muda, ili kuhakikisha maandalizi ya kikao hicho yanakamilika kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa
Bi. Devota amesema maandalizi hayo yanahitaji uratibu wa karibu miongoni mwa wadau, hususan katika kuhakikisha taarifa, nyaraka na maeneo yote muhimu yatakayojadiliwa yanaandaliwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika
Katika kikao hicho, wajumbe kutoka Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake pamoja na wadau wamepitia hatua zilizofikiwa katika maandalizi, kugawana majukumu na kujadili maeneo yanayohitaji kukamilishwa kabla ya mkutano. Aidha, msisitizo umewekwa katika upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa mipango, miradi na shughuli mbalimbali za sekta ya uchukuzi
Kikao cha 19 cha Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi kinatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 18 Novemba 2026 jijini Mwanza, ambapo wadau watapata fursa ya kutathmini utekelezaji wa mipango na shughuli za sekta, kubaini mafanikio na changamoto, pamoja na kujadili hatua za kuimarisha utendaji wa sekta ya uchukuzi
Maandalizi hayo yanaendelea kwa ushirikiano wa taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi, kwa lengo la kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa ufanisi na unazalisha mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa mipango na maendeleo endelevu ya sekta ya uchukuzi nchini ikiwa ni sehemu ya hatua za kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa kisekta, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali imeanza utekelezaji rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyoanza Julai 2026.
