Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SEKTA BINAFSI YAHIMIZWA KUWEKEZA USAFIRI WA ANGA

Imewekwa: 01 Oct, 2026
SEKTA BINAFSI YAHIMIZWA KUWEKEZA USAFIRI WA ANGA

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amehimiza Sekta Binafsi kuongeza uwekezaji katika usafiri wa anga ili kuimarisha huduma, kuongeza ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri Mhe. Kihenzile ametoa rai hiyo Septemba 29, 2026, alipokagua maendeleo ya maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ikiwemo Jengo la Watu Mashuhuri la Uhuru ambalo sehemu yake imekamilika na kuanza kutoa huduma.

Naibu Waziri Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika viwanja vya ndege nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Rehema Myeya, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za maboresho ya kiwanja hicho na Viwanja vingine Nchini lengo likiwa kuhakikisha Abiria wanapata Huduma za viwango.

“Uwekezaji huu wa Serikali umeleta maboresho makubwa katika miundombinu na huduma za uwanja. Tunaendelea kuona matokeo chanya yanayoongeza ufanisi wa KIA na kuboresha huduma kwa wasafiri,” amesema Mhandisi Myeya.