Wizara ya Uchukuzi kuzindua sera mpya ya sekta mwishoni mwa mwaka

Wizara ya Uchukuzi imesema kuwa mwishoni mwa mwaka huu itazindua sera mpya ya Uchukuzi kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2035, huku wadau wakihimizwa kuhakikisha inajibu mahitaji ya sasa na mabadiliko ya teknolojia.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika kikao cha wadau na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, Katibu Mkuu Profesa Godius Khayarara alisema sera hiyo inalenga kuboresha na kudumisha miradi ya uchukuzi kwa muda mrefu.
“Katika sera hii lazima tuangazie kujenga na kufanya maboresho makubwa na madogo ili miradi yetu iweze kudumu kwa miaka mingi. Hivyo teknolojia pamoja na wafanyakazi imara wanahitajika katika kuboresha miundombinu,” alisema Prof. Khayarara.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Ludovick Nduhiye, alisema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya uchukuzi hivyo ni muhimu kwa wataalamu kuhakikisha sera mpya inatoa mwelekeo wa usimamizi na uendelezaji wa uwekezaji huo.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Maseke Mabiki, alibainisha kuwa uandaaji wa sera hiyo umezingatia ushirikishwaji wa makundi yote muhimu yakiwemo wadau wa sekta binafsi na taasisi zote chini ya wizara.
Naye Mratibu wa maandalizi ya sera hiyo, Dk. Josephat Kweka, aliahidi kuwa maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau wote yatazingatiwa ili kuhakikisha sekta ya uchukuzi inasimamiwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya Watanzania.