Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

UJENZI WA MATENKI 15 YA KUHIFADHIA MAFUTA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA BIASHARA YA NISHATI KIKANDA

Imewekwa: 04 Mar, 2026
UJENZI WA MATENKI 15 YA KUHIFADHIA MAFUTA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA BIASHARA YA NISHATI KIKANDA

Serikali imesema kukamilika kwa ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta katika eneo la Kigamboni, Jijini Dar es salaam ni hatua ya kimkakati ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji wa nishati kikanda na kimataifa.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo tarehe 03 Machi,2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema nafasi ya kijiografia ya Tanzania inaipa fursa ya kuwa lango kuu la kuhudumia nchi zisizo na bahari kikanda

Amesema maboresho yanayoendelea kufanyika katika bandari za Bahari ya Hindi, maziwa makuu na bandari kavu ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa taifa, sambamba na kuimarisha ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa miundombinu hiyo.

Dkt. Samia ameeleza kuwa uamuzi wa kushirikisha sekta binafsi ulikuwa wa kimkakati na umechangia kupunguza gharama za uendeshaji wa bandari na kuongeza ufanisi, huku fedha zinazopatikana zikielekezwa katika miradi mingine ya maendeleo ikiwemo mradi huu wa matenki ya mafuta.

Ameongeza kuwa maboresho katika sekta ya uchukuzi yameongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa na kuongeza ushindani wake kimataifa, huku ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ukitarajiwa kupanua zaidi uwezo wa nchi kupokea meli za ukubwa wowote.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof.Makame Mbarawa, amesema kuwa mradi huo utaongeza uwezo wa bandari katika kuhudumia shehena ya mafuta na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji wa mizigo kwa nchi jirani na kubainisha kuwa maendeleo ya bandari kavu ikiwemo ile ya  Kwala, Dodoma, Morogoro na Shinyanga yamepunguza msongamano bandarini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa  TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema mradi huo wa Sh bilioni 678.6 utakamilika Februari 3, 2027 baada ya mkataba wa miezi 24, na kwa sasa umefikia asilimia 21 ya utekelezaji na kuongeza kuwa mradi huo utawezesha kupokea petroli, dizeli na mafuta ya ndege, huku awamu ya pili ikihusisha ujenzi wa magati mapya ili kuongeza ushindani wa bandari ya Dar es Salaam kuvutia meli za kimataifa.