NIT YATAKIWA KUSIMAMIA TAFITI
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameliagiza Baraza la 13 la Uongozi la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuhakikisha linasimamia kikamilifu mafunzo na tafiti zinazolenga kutatua changamoto za sekta ya usafirishaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Agizo hilo amelitoa wakati wa uzinduzi wa baraza hilo Mkoani Morogoro na kusisitiza kuwa chuo kina wajibu mkubwa wa kusaidia Serikali kuandaa sera madhubuti za uchukuzi.
Waziri Prof. Mbarawa amesema utekelezaji wa jukumu hilo utawezesha chuo kufikia malengo ya mpango wake wa miaka mitano wa kuboresha ubora wa elimu na mafunzo, kukidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa na kuimarisha miundombinu ya kujifunzia ikiwemo maabara, maktaba na teknolojia za kisasa.
Aidha, ameongeza kuwa maandalizi ya awali ya Sera Mpya ya Taifa ya Uchukuzi yamezingatia njia mpya za usafiri kama Cable Transport na Space Transport, hivyo akalitaka baraza hilo kuandaa mafunzo yatakayozalisha wataalamu katika maeneo hayo yanayoibukia.
Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema katika miaka mitatu iliyopita chuo kimeanzisha kozi nane za kimkakati, zikiwemo za uzamili, shahada na stashahada. Pia kimeanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (CoEATO), kimenunua ndege mbili za mafunzo na kuanza kutoa mafunzo ya urubani kwa wanafunzi 22.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la 13 la Uongozi la NIT, Prof. Ulingata Mbamba amesema baraza hilo litaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya chuo, kuimarisha utawala bora na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa
