Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

PROF.MBARAWA ARIDHISHWA NA UJENZI CHUO CHA ANGA, ASISITIZA UBORA, VIWANGO NA KUAKISI THAMANI YA FEDHA

Imewekwa: 04 Mar, 2026
PROF.MBARAWA ARIDHISHWA NA UJENZI CHUO CHA ANGA, ASISITIZA UBORA, VIWANGO NA KUAKISI THAMANI YA FEDHA

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa  Tarehe 04 Machi, 2026 amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa majengo ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga nchini.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Prof.Mbarawa amesema ameridhishwa na maendeleo ya  mradi ambao mpaka sasa uko ndani ya mda na unaendelea kwa kasi inayotakiwa na kutaka ubora, ratiba, viwango vya kitaalamu na thamani halisi ya fedha kuzingatiwa

Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa kwenye sekta ya anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege karibu kila mkoa, ununuzi wa ndege na sasa  imejipanga kuendelea kuimarisha miundombinu ya mafunzo ya sekta ya anga ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu watakaokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.

“Mradi huu  unaotekelezwa kwa shilingi bil. 78 ambao sasa umefikia asilimia 10.3 ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini,tunasisitiza utekelezaji wake kuzingatia ubora, ratiba na viwango vya kimataifa, na kuakisi thamani halisi ya fedha ili chuo hiki kiwe kitovu cha mafunzo ya anga katika ukanda huu,” amesema Waziri Mbarawa.

Mwisho Prof.Mbarawa ametoa rai kwa TCAA kuhakikisha wanawapatia fursa ya mafunzo kwa vitendo vijana wa ndani wanaosoma masomo ya uhandisi na kusisitiza miradi yotr mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa ndani ya nchi itumike kama darasa kwa vijana wetu wanaojifunza ili kuzalisha wataalamu wengi wa ndani kwa maendeleo ya Taifa

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Salim Msangi amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Julai,2023 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa mamlaka hiyo wa kuimarisha uwezo wa ndani katika mafunzo ya anga, sambamba na kuendana na miongozo na matakwa ya mashirika ya kimataifa ya usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Mha. Stephen Mwakasasa, amesema ujenzi unaendelea vizuri kulingana na michoro na usanifu.