WAZIRI WA UCHUKUZI ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2025
Baada ya kuhudhuria ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025, uliofanywa na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ametembelea mabanda ya maonesho yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Prof. Mbarawa amepongeza ubunifu, juhudi na ushiriki wa taasisi, vijana, watafiti na wabunifu kutoka sekta ya uchukuzi na teknolojia kwa kuonesha namna uwezo wa kitaifa unavyokua katika kuendeleza mifumo ya usafiri rafiki kwa mazingira.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali, Prof. Mbarawa amesema “Maonesho haya yanaonesha wazi dhamira ya nchi yetu katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza ufanisi na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kwenye mifumo yetu ya usafirishaji. Serikali itaendelea kushirikiana na wabunifu na sekta binafsi ili kuharakisha mageuzi ya usafiri unaokwenda na mahitaji ya dunia ya sasa.”
Aidha, amewahimiza wananchi kufika Mnazi Mmoja kujifunza kuhusu teknolojia mpya, miradi ya usafiri endelevu, huduma za wizara, na fursa zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi na kuwataka wawekezaji binafsi kuchangamkia fursa sasa kuwekeza kwenye miradi ya uchukuzi maana milango iko wazi
Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Latra CPA Habibu Suluo ambaye ameelezea umuhimu wa usimamizi wa mifumo ya usafiri iliyo salama, bora na endelevu
Amesema mamlaka itaendelea kusimamia matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuhimiza matumizi ya nishati safi kama njia ya kuongeza ufanisi wa Sekta ya Uchukuzi na kutunza mazingira
Maonesho haya yaliyoanza tarehe 24 November, 2025 yenye kaulimbiu ya " Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji" yataendelea hadi tarehe 29 Novemba 2025.
