Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

WAZIRI WA UCHUKUZI AHIMIZA KASI MRADI UWANJA WA NDEGE MSALATO

Imewekwa: 31 Jan, 2025
WAZIRI WA UCHUKUZI AHIMIZA KASI MRADI UWANJA WA NDEGE MSALATO

Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amehimiza wasimamizi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato ambao ni TANROADS na TAA  kuhakikisha Mkandarasi anaongeza kasi zaidi ya umaliziaji wa hatua zilizobaki ili kukabiliana na mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha

Mbarawa ameyasema hayo  wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege kilichopo Msalato Jijini Dodoma iliyofanyika Tarehe 30 Januari,2025

"Ninaipongeza  hatua zilizofikiwa nimeona sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa uwanja wa kurukia na kutua ndege unaogharimu shilingi Bil 165.65  kazi inaendelea vizuri na  imefikia asilimia 84 natoa rai msimamieni Mkandarasi aongeze kasi hapa ili mvua zinazotarajiwa kuanza mwezi ujao zisimkwamishe" amesisitiza Mbarawa

Amesema Mkandarasi asimamiwe vyema afanye kadri awezavyo na kwa thamani halisi ya fedha uwekaji wa rami umalizike ndani ya wiki mbili sababu mwezi wa tatu kutakuwa na mvua nyingi na huwezi kuweka rami wakati wa mvua

Aidha ameongeza kuwa kazi zitakazobaki za kufunga mifumo ya kuongozea ndege sambamba na sehemu ya pili ya ujenzi wa jengo la abiria ambao umefikia asilimia 70 ambavyo vinaweza kufanywa taratibu hata kipindi cha mvua vitakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2025 na uwanja utakuwa tayari kwa matumizi ambapo utaleta tija kwa Nchi na wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani

Akitoa taarifa za mradi Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma Mha Zuhura Amani amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri  ambapo ujenzi wa uwanja umefikia asilimia 84, na upande wa majengo yote unaohusisha jengo la kushukia na kupandia abiria na jengo la kuongozea ndege  vimefikia asilia 51 kwa ujumla na wataongeza kasi ya usimamiaji ili vikamilike kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha ili wananchi waanze kukivunia maendeleo yanayoletwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhi Hassan