Waziri Prof. Mbarawa aipongeza Bodi na Menejimenti ya NIT

Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amefungua Rasmi Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Usafirishaji, Logistiki na Usimamizi umefunguliwa rasmi tarehe 21 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Mkutano huo wa siku mbili, unaoendelea hadi tarehe 22 umeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa lengo la kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini na kimataifa.
Katika hotuba ya ufunguzi, Waziri Mbarawa amekipongeza Chuo cha NIT kwa kuandaa kongamano hilo muhimu, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na taasisi katika kukuza sekta ya usafirishaji.
Ameeleza kuwa serikali imepanga kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 50 katika kituo cha mafunzo ya vitendo (Center of Excellence) kitakachojengwa katika Chuo cha NIT, kwa lengo la kutoa mafunzo ya hali ya juu kwa wataalamu wa sekta ya usafirishaji.
Aidha, Waziri Mbarawa ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo uzinduzi wa treni ya kisasa ya umeme (SGR) hivyo Mbarawa Amemshkuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo hayo.
Waziri amewahimiza washiriki wa mkutano huo, wakiwemo wageni kutoka mataifa mbalimbali, kutumia fursa ya uwepo wao nchini kutembelea vivutio vya utalii kama Serengeti na Zanzibar, ili kujionea uzuri wa Tanzania na kuchangia katika kukuza sekta ya utalii.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Dkt. Prosper Mgaya amesema chuo hicho kimekuza taaluma ya usafirishaji pia kuleta mabadiliko katika usafiri wa anga, barabara, reli na majini, na hivyo kurahisisha huduma kwa wananchi na kuleta tija kiuchumi.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Ulingeta Mbamba, ambaye ni na mmoja wa wazungumzaji wakuu, amezungumzia umuhimu wa utafiti na ubunifu katika kuboresha mifumo ya usafirishaji.
Kaulimbiu ya mkutano huu ni "Kuvuna Mifumo ya Usafiri ya Ubunifu na Endelevu kwa Uboreshaji wa Uhamaji na Usalama" ikilenga kuhimiza matumizi ya teknolojia na uongozi bora katika sekta ya usafiri wa anga.