Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu kuzindua meli ya MV. Mwanza

Imewekwa: 22 Jan, 2026
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu kuzindua meli ya MV. Mwanza

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuzindua meli mpya ya kisasa ya MV New Mwanza kesho Ijumaa, tarehe 23 Januari, 2026, katika Bandari ya Mwanza Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Mwanza, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema meli hiyo imejengwa na mkandarasi kutoka Korea, Gas Entec Ship-Building, kwa kushirikiana na TASHICO kwa gharama ya shilingi bilioni 120.56.

Ameeleza kuwa meli hiyo imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na imefanya safari sita za majaribio katika ruti ya Mwanza–Bukoba tangu Machi 2025, ambapo matokeo yake yameridhisha na TASAC imeruhusu kuanza rasmi kwa safari.

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa meli hiyo ya ghorofa nne ndiyo kubwa zaidi katika ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa matatu kwa wakati mmoja.

Kabla ya uzinduzi, Waziri Mkuu atafanya ziara ya kikazi kukagua Mradi wa Kituo cha Kimataifa cha Kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MLVMCT) katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela, ili kujionea maandalizi na uwezo wa kukabiliana na dharura.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amewakaribisha wananchi kushiriki tukio hilo kuanzia saa 2 asubuhi, na kueleza kuwa Waziri Mkuu pia ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa matenki ya maji, vituo vya kusukuma maji na mabomba makuu katika Mtaa wa Sahwa, Kata ya Kwahnima, jijini Mwanza.