Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

WAZIRI MBARAWA, KIHENZILE WASHUKURU WATUMISHI WA WIZARA YA UCHUKUZI

Imewekwa: 19 Nov, 2025
WAZIRI MBARAWA, KIHENZILE WASHUKURU WATUMISHI WA WIZARA YA UCHUKUZI

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameishukuru Menejimenti, Watumishi na Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Uchukuzi kwa kufanya kazi kwa weledi na bidii Hali iliyofanya Waziri hiyo na Naibu Waziri, David Kihenzile, kuaminiwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza wizara hiyo kwa awamu ya pili.

Akizungumza leo mara baada ya kupokelewa rasmi katika ofisi za wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Profesa Mbarawa alisema kurejea kwao katika wizara kunatokana na kazi kubwa iliyofanywa na watumishi bila kuchoka.

“Kama msingefanya kazi usiku na mchana na matokeo kuonekana, ingekuwa vigumu sisi kurudi tena hapa. Kila kada na kila mtumishi amechangia kwa sehemu yake,” alisema Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri David Kihenzile aliwataka watumishi kuendeleza ushirikiano waliouonyesha katika kipindi kilichopita, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ndio nguzo muhimu ya kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, aliwakaribisha viongozi hao huku akieleza kuwa kurejea kwao kunatoa hamasa mpya kwa wizara, na kuahidi kuwa menejimenti itaendelea kushirikiana nao kuboresha sekta ya uchukuzi.

Prof. Mbarawa na Kihenzile waliapishwa rasmi leo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.