Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Waziri Mbarawa ataka Kasi Ujenzi SGR Mwanza-Isaka

Imewekwa: 22 Feb, 2025
Waziri Mbarawa ataka Kasi Ujenzi SGR Mwanza-Isaka

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutumia uzoefu wa uendeshaji wa reli ya SGR Dar Es Salaam - Dodoma katika kufanya maboresho kwenye ujenzi wa reli ya SGR kipande cha tano (Lot 5) Isaka - Mwanza ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo alipotembelea mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi huo wa kisasa unaotarajiwa kuleta mapinduzi katika nyanja ya usafiri na usafirishaji nchini.

" Tunataka yale tuliyojifunza kule hapa yasijirudie tena, kwa mfano Dar es Salaam kuna changamoto ya maegesho ya magari pamoja na Dodoma sasa kwenye mikoa hii tuhakikishe tunajipanga vizuri hata watu wakiongezeka kusiwe na shida," Amesema Mbarawa.

Aidha Waziri Mbarawa amesema kwa upande wa serikali watahakikisha wanamsimamia vizuri mkandarasi pamoja na kumpatia malipo kwa wakati ili mradi huo ukamilike kwa wakati na wananchi wanufaike kama Dar es salaam, Morogoro na Dodoma wanavyonufaika.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, moja ya mkoa unaonufaika na mradi huo Kenani Kihongosi amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na tija kubwa kwa wananchi ikiwemo fursa za kibiashara na kuvutia wawekezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa mradi huo unaogharimu kiasi cha shilingi trilioni 3.06 umefikia aslimia 63.04 ambapo amesema hali ya mvua ilikwamisha mradi huo lakini kwa sasa wanakwenda kwa kasi inayotakiwa.

Pia Kadogosa amesema kuwa kama sehemu ya maboresho zaidi watahakikisha wanajenga makazi kwa ajili ya wasimamizi wa vituo vya polisi vilivyopo katika stesheni zinazojengwa jambo ambalo halikufanyika katika sehemu ambazo SGR imeanza kazi.