Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

WAZIRI MBARAWA APIGILIA MSUMARI IDADI YA MABAHARIA WANAWAKE

Imewekwa: 24 Oct, 2023
WAZIRI MBARAWA APIGILIA MSUMARI IDADI YA MABAHARIA WANAWAKE

Serikali imezielekeza taasisi zote zinazosimamia usafiri wa Majini kushirikiana na kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya mabaharia wanawake ili kuwapa fursa ya kunufaika na Sekta ya Bahari ndani na nje ya nchi.  

 

Kauli hii imetolewa Kusini Pemba na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa wakati alipofungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani na kusema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa meli ambapo itakapokamilika mahitaji ya mabaharia yataongezeka.

 

‘Leo tunaadhimisha siku ya bahari lakini tukitafuta takwimu hapa tutagundua idadi ya maharia wanawake ni ndogo sana, taasisi husika wekeni mikakati madhubuti idadi hii iongezeke ikiwekana siku za mbeleni tuone mabaharia wanawake kutoka bara na visiwani’ amesema Waziri Mbarawa.

 

Waziri Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) kwa kukamilisha utafiti wa vyombo vya majini uliofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa lengo la kujua idadi ya vyombo hivyo nchini.

 

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amesema asilimia 90 ya bidhaa inayosafishwa kupitia njia ya maji inaweza kuimarishwa zaidi kwa kuzingatia sheria na kanuni na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kusafirisha mzigo mwingi zaidi na kwa usalama.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Khadija Khamis amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ili kuhakikisha sheria zinazoongoza usafiri wa majini kimataifa zinazingatiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira wa WIzara ya Uchukuzi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Stela Katondo amesema miongoni mwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa sasa ni kutoa elimu kwa wadau hususani kwa chagamoto zinazoweza kujitokeza kwa uharibifu unaofanywa kupitia utupaji wa taka ngumu na nyepesi katika bahari na maziwa nchini.

 

Maadhimisho ya Siku ya Bahari kwa mwaka 2023 yanaadhimishwa kitaifa Mkoa wa Kusini Pemba yamebeba kauli mbiu inayosema “Miaka 50 ya MARPOL Uwajibikaji Wetu Unaendelea’ yafunguliwa 25 Septemba na yanatarajiwa kuhitimishwa 28 Septemba 2023.