WAZIRI MBARAWA AITAKA TPA KUONDOA VIKWAZO BANDARI KIGOMA

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa bandari katika Ziwa Tanganyika kuondoa vikwazo visivyo na sababu kwa wafanyabiashara wanaotumia Ziwa hilo kusafiririsha mizigo mbalimbali kwani wengi wameonyesha nia ya kutumia ziwa hilo kibiashara.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo leo alipotembelea bandari ya Kigoma ili kujionea maendeleo ya kiutendaji katika bandari za Ziwa Tanganyika.
" Makampuni mengi ya madini kutoka nchini DRC yameonyesha dhamira ya kupitishia mzigo wake bandari ya Kigoma au Karema kwa maana ya kuingiza kutoka nje ya nchi kupitia bandari ya Dar Es Salaam au kutoa Kongo kwenda bandari ya Dar Es Salaam," Amesema Mbarawa.
Pia Prof. Mbarawa amesema wao kama sekta ya uchukuzi watajitahidi kuhakikisha wanaweka sera nzuri zitakazowavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutumia reli na bandari ili kufikia azma ya kurahisisha biashara na nchi jirani.
Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Juma Kijavara amesema kwa sasa wako kwenye mazungumzo na nchi ya Japan kwa ajili ya uboreshaji wa bandari ya Kigoma pamoja na ujenzi wa njia za kuingia bandarini hapo.
Aidha Kijavara amesema kuwa katika jitihada za kuboresha shughuli za kibiashara baina ya Tanzania na nchi jirani btauari TPA imekabidhi eneo kwa kampuni ya uchimbaji madini kutoka nchini Kongo katika Bandari ya Karema, kampuni ambayo inakisudia kujenga meli ya mizigo itakayokuwa ikifanya kazi katika Ziwa Tanganyika.