Waziri Mbarawa aipongeza TPA Ujenzi wa Matenki ya Mafuta

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa ( Mb) ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kuwasimamia vyema Makandarasi wanaojenga mradi wa kikamkati wa matenki maalum ya kuhifadhi na kusambaza mafuta ( Oil Terminal) ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza tarehe 19 Februari,2025 baada ya kutembelea mradi huo unaojengwa katika kata ya Tundwi, wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Mbarawa amesema ni muhimu mradi huo ukasimamiwa ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora kwani kukamilika kwake kutasaidia kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza kwa kiwango kikubwa foleni ya Meli za kupakua mafuta.
“ Mara ya mwisho nilipokuja hapa mwezi Septemba mwaka jana mradi huu ulikuwa asilimia 5 tu na sasa umefikia asilimia 14.77. Hakika kazi inaenda vizuri n inaonekana, muhimu ni kwa Makandarasi hawa kuongeza bidii, kufanya kazi kwa ubora na mradi huu ukamilike kwa wakati ,” amesema Mhe. Prof. Mbarawa
Amesema Serikali imeamua kujenga matenki hayo 15 ya kuhifadhi na kusambaza mafuta yenye ujazo wa mita za ujazo 378,000 ili kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kiwa moja ya Bandari zenye ushindani duniani pia kukabiliana na uhaba wa mafuta unaoweza kutokea.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema mradi huo unaojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 678.6 kwa sasa umefikia Asilimia 14.77 tangu ulipoanza Agosti 16,2024 na utasimamiwa vyema na kumalizika kwa wakati ndani ya miaka miwili kwa mujibu wa mkataba na kuwa na tija kwa bandari ya Dar es Salaam na Serikali kwa ujumla katika kukusanya kodi na tozo mbalimbali.
“ Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ya kuhimiza utendaji na kimsingi ameridhika na kazi inayofanyika hapa na amehimiza ifanyike kwa bidii na mradi ukamilike kwa wakati, tumepokea maelekezo na tutayatekeleza,” amesema Dkt. Mdima.
Mradi huo wa Matenki 15 ya kuhifadhi na kusambaza mafuta, utahusisha matenki sita ya kuhifadhi mafuta ya Diseli, matenki matano ya kuhifadhia mafuta ya petroli, matenki matatu kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ya Kuendeshea ndege na tenki moja litakuwa la ziada likitumika kupitishia mafuta( Interface tank).