WANASAYANSI KUTOKA NCHI 53 WAKUTANA ARUSHA KUJADILI MABADILIKO YA TABIANCHI – PROFESA MBARAWA
Wanasayansi kutoka takribani nchi 53 duniani wamekutana jijini Arusha katika Mkutano wa Tatu wa Waandishi Wakuu wa Kundi la Kwanza la Jopo la Serikali za Nchi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), kujadili mchango wa sayansi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema taarifa sahihi za kisayansi na huduma za tahadhari za mapema ni muhimu katika kupanga, kusanifu na kujenga miundombinu imara inayoweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Profesa Mbarawa amesisitiza kuwa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na tabianchi yanapaswa kupewa kipaumbele katika mipango na uwekezaji wa muda mrefu, hususan katika sekta ya uchukuzi inayokabiliwa na athari za mvua kubwa, mafuriko, joto kali na dhoruba. Ameongeza kuwa taarifa hizo zitasaidia taasisi na wadau kufanya maamuzi sahihi katika kubuni na kuendeleza miundombinu himilivu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema hali ya hewa na tabianchi havitambui mipaka ya kisiasa, hivyo kukabiliana na athari zake kunahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali, jamii, wanasayansi na mataifa. Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha huduma za tahadhari za mapema ili kulinda maisha ya wananchi, mali na miundombinu.
Naye Mwenyekiti wa IPCC, Profesa Sir Jim Skea, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Arusha na TMA kwa ushirikiano na dhamira yao katika kufanikisha mkutano huo, akieleza kuwa juhudi hizo zinaimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya sayansi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo unaofanyika kuanzia Novemba 2 hadi 6, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha PAPU jijini Arusha, umeandaliwa na IPCC kwa kushirikiana na TMA. Lengo lake ni kuimarisha mchango wa Kundi la Kwanza katika maandalizi ya Taarifa ya Saba ya Tathmini ya IPCC (AR7), inayotathmini misingi ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuongeza ushiriki wa wanasayansi wa Afrika katika michakato ya kisayansi ya kimataifa.
