SHILINGI BILIONI 11 ZAFUNGUA FURSA MPYA ZA USAFIRI WA ANGA ARUSHA – PROFESA MBARAWA
Serikali imewekeza takribani Sh bilioni 11 kuboresha Uwanja wa Ndege wa Arusha, hatua iliyowezesha kuanza kwa huduma za ndege saa 24 kwa siku, siku saba za wiki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hizo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hatua hiyo itaongeza fursa za biashara, uwekezaji na utalii, pamoja na kurahisisha safari za wananchi.
Amesema awali uwanja huo ulikuwa ukitoa huduma kwa saa 12 pekee, lakini uwekaji wa taa ulioanza mwaka wa fedha 2023/2024 umewezesha ndege kuruka na kutua mchana na usiku.
Amewataka TAA kushirikiana na mashirika ya ndege kuongeza safari na kuhakikisha uwekezaji huo unaongeza matumizi ya uwanja na mapato, huku TCAA ikiendelea kusimamia viwango vya usalama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mambokaleo, amesema mamlaka hiyo imejipanga kuongeza watumishi na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kutoa huduma kwa ufanisi saa 24.
Naye mfanyabiashara Davis Mosha amesema huduma hizo zitarahisisha safari za kibiashara, kuokoa muda na kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara wanaohitaji kusafiri nyakati tofauti.
