Wananchi wa Serengeti kulipwa fidia
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile imewahakikishia wananchi wa Serengeti mkoani Mara waliofanyiwa uthamini ili kupisha ujenzi wa kiwanja cha ndege kuwa fidia zao zitalipwa mapema iwezekanavyo kabla ya ujenzi kuanza.
Kihenzile ameyasema hayo alipofanya ziara kujionea mahali Kiwanja cha ndege cha Serengeti kitakapojengwa ambapo alikutana na wananchi waliokuwa wakimsubiri ili kueleza kero yao ya fidia.
“Mimi niwaombe muondoke mkiwa kifua mbele kwani serikali yenu inawajali na haiwezi kuruhusu mkandarasi aanze kazi kabla hamjalipwa fidia, na nataka mjue tenda ya ujenzi imeshatangazwa na hivi karibuni mkandarasi atapatikana,” Amesema Kihenzile.
Aidha Kihenzile amesema kuwa kiwanja hicho cha ndege ikinatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vikubwa nchini maalum kwa ajili ya kuchochea eneo la utalii hususan eneo la kanda ya ziwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Angelina Lubela amesema kuwa wananchi wa Serengeti wanasubiria kwa hamu kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja hicho ambacho kwa namna moja ama nyingine utasaidia kukuza uchumi wa wananchi na Wilaya kwa ujumla.
