Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KITUO CHA KURASINI KUANZA KUHUDUMIA MIZIGO NOVEMBA, KUPUNGUZA MSONGAMANO BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 26 Aug, 2026
KITUO CHA KURASINI KUANZA KUHUDUMIA MIZIGO NOVEMBA, KUPUNGUZA MSONGAMANO BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Kituo cha Lojistiki cha Kurasini kinachojengwa katika eneo la zamani la EPZA, Dar es Salaam, kinatarajiwa kuanza rasmi kuhudumia makasha ya mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam mwezi Novemba mwaka huu

Prof. Mbarawa amesema hayo leo Agosti 21,2026,wakati akikagua maendeleo ya Mradi wa Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam katika eneo hilo, akieleza kuwa kituo hicho kitasaidia kupunguza msongamano wa makasha na malori bandarini, huku kikirahisisha utoaji wa mizigo kwa wafanyabiashara

Prof.Mbarawa amesema TPA, TRA na taasisi nyingine za Serikali zitakuwepo Kurasini ili huduma za uhakiki, ukaguzi na utoaji wa mizigo zifanyike kwa ufanisi. Pia, kituo hicho kitawekewa mashine za scanning kwa ajili ya ukaguzi na usalama wa mizigo

Aidha, Prof. Mbarawa amesema Serikali imekubaliana na TPA kuangalia uboreshaji na uunganishaji wa barabara kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Kurasini, kwa kushirikiana na TANROADS na TARURA, ili kuwezesha mizigo kusafirishwa moja kwa moja kwenda katika kituo hicho

Amesema awamu ya kwanza ya kituo hicho itakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 150,000, huku awamu ya pili ikikamilika uwezo ukifikia makasha 700,000 kwa mwaka, hatua itakayoongeza nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia shehena zaidi

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema ongezeko la shehena limeifanya Serikali kuongeza miundombinu ya kuhifadhia mizigo nje ya eneo kuu la bandari. Alisema Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inahudumia zaidi ya makasha milioni 1.3 kwa mwaka

Abed amesema ujenzi wa Kurasini Lojistiki Centre umefikia asilimia 98 na kukamilika kwake kutapunguza msongamano wa makasha bandarini, kuongeza ufanisi wa utoaji wa mizigo, kupunguza muda wa makasha kukaa bandarini na kuimarisha uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia biashara za ndani na kimataifa.