Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

WANAFUNZI 23 WA TANZANIA WATIKISA MISRI KWA NIDHAMU, WAZIRI MBARAWA AFARIJIKA

Imewekwa: 05 Oct, 2026
WANAFUNZI 23 WA TANZANIA WATIKISA MISRI KWA NIDHAMU, WAZIRI MBARAWA AFARIJIKA

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema amefarijika na kujivunia heshima kubwa inayoletwa na wanafunzi 23 wa Kitanzania wanaosoma Chuo cha Kimataifa cha Arab Academy for Science, Technology and Maritime Transport (AASTMT) nchini Misri kutokana na nidhamu na ufaulu wao wa hali ya juu.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo jana jijini Alexandria wakati alipofanya ziara rasmi chuoni hapo na kukutana na kundi la wanafunzi hao wanaosomea fani za Uhandisi wa Meli, unahodha na biashara ya kimataifa, logistiki ya usafiri wa majini .

Akizungumza na wanafunzi hao  baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya wanafunzi hao kutoka kwa uongozi wa chuo, Waziri Mbarawa aliwapongeza wanafunzi hao na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wema wa taifa.

Kwa upande wake, Rais wa Chuo hicho Prof Ismail AbdelGhafar Farag amesema kuwa anaridhishwa na mwenendo wa wanafunzi wa Tanzania, ambao amewataja kuwa ni mfano wa kuigwa chuoni hapo.

"Wanafunzi hawa ni wenye nidhamu na Wanajituma kwa bidii masomoni na wanaheshimu miongozo yote ya chuo. Ndiyo maana matokeo yao ni mazuri kila wakati. Tunawapongeza sana," alisema Rais huyo.

Naye mmoja wa wanafunzi hao Ngudu Pasiano Nemes anayesomea fani ya Uhandisi wa Meli alisema wanafurahia mazingira ya masomo na namna wanavyotendewa vizuri na waalimu wao, jambo ambalo limekuwa chachu ya mafanikio yao.

"Tunatendewa vizuri hapa na tunapewa kipaumbele cha kutosha. Mazingira mazuri na upendo wa waalimu wetu ndio siri ya matokeo yetu mazuri. Tutaendelea kusoma kwa bidii ili tukareje nyumbani tukaitumikie nchi yetu," alisema mwanafunzi huyo.

Chuo cha AASTMT ni miongoni mwa vyuo vinavyoongoza duniani katika fani za baharini, na uwepo wa wanafunzi 23 wa Tanzania hapo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wanafunzi hao 23 pamoja na wengine wawili kutimiza idadi ya wanafunzi 25, wote wanasomeshwa na TPA kwa niaba ya Serikali na wamepewa ajira ya kudumu na TPA.