Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

TRC NA WCF WASAINI MAKUBALIANO KUONGEZA THAMANI YA SGR

Imewekwa: 05 Oct, 2026
TRC NA WCF WASAINI MAKUBALIANO KUONGEZA THAMANI YA SGR

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mikutano na hoteli katika Stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete, Morogoro.

Hafla hiyo imeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu.

Akitoa salama katika hafla  hiyo Waziri Mhe. Sangu ameipongeza TRC na WCF kwa kushirikiana katika mradi huo kwani Ushirikiano huo unadhihirisha umuhimu wa Taasisi kutumia rasilimali zilizopo ili kuboresha Huduma na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Waziri Mhe. Sangu ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia WCF imeanza kuwekeza kwenye Ujenzi wa Miundombinu ikiwa ni hatua ya kutanua wigo wa Uwekezaji.

Naye Naibu Waziri Mhe. Kihenzile amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya reli, ikiwemo SGR, iliyoboresha usafirishaji wa abiria na mizigo na kuimarisha muunganiko wa maeneo nchini.

Amesema mtandao wa reli wenye zaidi ya kilomita 2,000 unapaswa kutumika kwa ufanisi ili kuongeza tija na thamani ya maeneo yanayomilikiwa na Serikali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, Mhe. Kihenzile ametoa wito kwa sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika reli, bandari na viwanja vya ndege kuwekeza zaidi na kuongeza thamani ya miundombinu ya uchukuzi.