Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

WAFANYABIASHARA WAIPOKEA AIR TANZANIA LAGOS

Imewekwa: 23 Sep, 2025
WAFANYABIASHARA WAIPOKEA AIR TANZANIA LAGOS

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imezindua rasmi safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Lagos, hatua inayounganisha Afrika Mashariki na Magharibi kupitia sekta ya anga. Hafla ya uzinduzi ilifanyika jijini Lagos tarehe 20 Septemba 2025, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali wa Tanzania na Nigeria, wadau wa biashara na utalii pamoja na wanadiaspora.

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Mhe. Selestine Kakele, alisema: “Huu ni mwanzo wa sura mpya na ni daraja  linalounganisha mataifa mawili makubwa na yenye ushawishi katika Bara la Afrika kupitia majiji yake mawili, jiji la Lagos, Nigeria na Dar es Salaam, Tanzania.”

Kwa upande wake, Waziri wa Usafiri wa Anga na Maendeleo Nigeria, Mhe. Festus Keyamo, aliyewakilishwa na Bi. Janet Oputa, alisisitiza kuwa safari hizi zitachochea biashara, utalii na mawasiliano ya kitamaduni, sambamba na kutekeleza Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Soko Moja la Usafiri wa Anga Afrika (SAATM).

Akiongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, alisema: “Nigeria ni taifa la pili kwa ukubwa wa uchumi barani Afrika baada ya Afrika Kusini. Hata hivyo, katika sekta nyingine, Egypt inashika nafasi ya pili baada ya Afrika Kusini. Kwa hiyo, tunaona hii kama fursa kubwa ya kuifungua nchi yetu kwa kuunganisha Tanzania na Nigeria kupitia huduma za usafiri wa anga.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mha. Peter Ulanga, alisema: “Kwa kuongeza kituo cha Lagos kwenye mtandao wa safari za Air Tanzania, inafanya ATCL kuhudumia takribani vituo zaidi ya 29 kwa safari za ndani na nje ya Tanzania. “Kwetu hii si uzinduzi tu wa safari, bali ni muendelezo wa mkakati wetu wa kibiashara wa kufungua nchi, kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wetu.”

Safari za Lagos zitafanyika mara tatu kwa wiki: Jumatatu, Jumatano, Ijumaa kutokea Dar es Salaam na Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, kutokea Lagos.