Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Uwekezaji Bandari ya Kisiwa Mgao kufungua fursa Ushoroba wa Kusini

Imewekwa: 11 Feb, 2026
Uwekezaji Bandari ya Kisiwa Mgao kufungua fursa Ushoroba wa Kusini

Serikali imesema uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 157 uliowekwa katika Bandari ya Mtwara na Bandari mpya ya Kisiwa Mgao unalenga kufungua na kuimarisha ushoroba wa Kusini, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara na uchumi katika ukanda huo pamoja na nchi jirani.

Kauli hiyo imetolewa Februari 11, 2026 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile ( Mb) , alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Bandari mpya ya Kisiwa Mgao pamoja na maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Mtwara.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kimkakati katika miundombinu ya bandari ili kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza gharama za usafirishaji na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta za viwanda, kilimo na madini. Ameeleza kuwa maboresho hayo yataifanya Bandari ya Mtwara na Kisiwa Mgao kuwa lango muhimu la biashara kwa mikoa ya Kusini na nchi za SADC.

“Nia ya Serikali ni kuhakikisha bandari hizi zinaunganishwa na miundombinu ya reli na barabara kwa kiwango cha kisasa ili kurahisisha usafirishaji wa shehena kutoka na kwenda bandarini. Hii itaongeza ushindani wa bandari zetu na kukuza mchango wake katika pato la taifa,” amesema Mhe. Kihenzile.

Aidha, ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, muda wa utekelezaji na thamani ya fedha katika kukamilisha kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mha.Erick Madinda, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amesema mradi wa ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao umefikia asilimia 33 ya utekelezaji wake na unaendelea vizuri kulingana na ratiba iliyopangwa.

Mha. Madinda ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapanua uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi ya mzigo mchafu na malighafi zake, hivyo kuifanya Bandari ya Mtwara na Kisiwa Mgao kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania.