UWEKEZAJI ATCL WAONYESHA MATOKEO CHANYA-NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye amesema kuwa kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kumesaidia kuimarika kwa Uchumi,utalii na mswala mbalimbali ya kijamii nchini
Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea makao makuu ya shirika hilo jijini Dar Es Salaam, kwa lengo la kujionea jinsi shirika hilo linavyofanya kazi pamoja na kujua changamoto mbalimbali zilizopo.
“Kabla ndege za ATCL hazijarejea gharama ilikuwa kubwa sana ya nauli na maeneo machache yalikuwa yanafikiwa lakini kwa sasa gharama ni kidogo hasa ukikata tiketi mapema na maeneo mengi yanafikiwa,” Amesema Nduhiye.
Pamoja na hayo Nduhiye amesisitiza uwezekano wa kuangalia upya kiwango cha nauli ili kuongeza abiria wengi zaidi kwani usafiri wa ndege ndiyo usafiri wa haraka zaidi na kila mtu angetamani kuutumia.
Awali akiwasilisha taarifa ya shirika hilo Mkuu wa Kitengo cha Mipango Kitula Yango amesema shirika hilo tangu lifufuliwe mwaka 2016 limepiga hatua katika maeneo mbalimbali ikiwemo ongezeko la abiria.
Yango amesema shirika hilo linahudumia abiria zaidi ya milioni moja kwa mwaka tofauti ilivyokuwa mwaka 2016/17 ambapo shirika hilo lilikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria laki moja kwa mwaka.
Aidha Yango ameongeza kuwa kwa sasa shirika Lina marubabi 118 ikilinganishwa na marubani 11 waliokuwepo shirika linapofufuliwa, huku wahandisi na mafundi ndege wakifikia 181 ukilinganisha na 27 waliokuwepo awali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Mhandisi Ladslaus Matindi amemshukuru Naibu Katibu Mkuu Ludovic Nduhiye kwa kutembelea shirika hilo na kuahidi kufanyia kazi ushauri na maoni aliyoyatoa ili kuongeza ufanisi.