USHIRIKIANO WA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI WAIFUNGUA BANDARI YA DAR ES SALAAM NA KUONGEZA UFANISI
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaendelea kuleta mageuzi chanya katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam,
Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo tarehe 09 Februari, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua huduma za makasha na kujionea hatua zilizofikiwa katika maboresho ya utoaji huduma bandarini.
Akiwa katika eneo la Kurasini, Profesa Mbarawa amesema ujenzi wa eneo jipya la kuhifadhia makontena lenye ukubwa wa mita za mraba 200,000 unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ufanisi wa bandari kwa kuongeza uwezo wa kupokea makontena kutoka 800,000 hadi 1,300,000 kwa mwaka.
Waziri Mbarawa, amesema maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa mizigo bandarini, kufungua bandari, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa, sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya reli inayoelekea Bandari Kavu ya Kwala na bandari nyingine.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema makusanyo ya mapato ya bandari yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Shilingi bilioni 700 hadi kufikia Shilingi trilioni 2, hatua inayodhihirisha matokeo chanya ya maboresho yanayoendelea.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus, amesema maboresho ya uendeshaji yameongeza uwezo wa kuhudumia makontena kutoka 18,000 mwaka 2024 hadi 36,000 mwaka 2025, akisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea utaendelea kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa bandari.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Uchukuzi wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maboresho katika sekta ya bandari, sambamba na kuhakikisha wadau wanazingatia wajibu wao katika kutoa huduma bora kwa maslahi mapana ya Taifa.
