Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

USALAMA WA WANANCHI NI KIPAUMBELE, SGR IENDELEE KUTOA HUDUMA MVUA AU JUA" WAZIRI MBARAWA

Imewekwa: 08 Oct, 2026
USALAMA WA WANANCHI NI KIPAUMBELE, SGR IENDELEE KUTOA HUDUMA MVUA AU JUA" WAZIRI MBARAWA

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuongeza maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino, ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya reli, huku akisisitiza usalama wa wananchi unapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza na uendeshaji wa huduma za reli nchini usisimame

Prof. Mbarawa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kikazi katika eneo la Kilosa–Gulwe mkoani Morogoro, leo tarehe 08 Oktoba,2026 ambapo amekagua maendeleo na hali ya miundombinu ya reli

Amesema TRC inapaswa kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo yote hatarish na kuchukua hatua za kuimarisha maeneo yenye changamoto kabla ya mvua kubwa kunyesha

“Kipaumbele cha kwanza kiwe usalama wa raia, tuhakikishe Watanzania wako salama muda wote, hatupaswi kusubiri miundombinu iharibike ndipo tuchukue hatua, maandalizi na kinga yamalizike mapema” amesema Prof. Mbarawa

Mbarawa ameipongeza TRC kwa kazi inayofanyika katika maeneo mbalimbali ya reli, akisema kila alipokagua ameshuhudia watendaji wakitekeleza majukumu yao na kuitaka TRC kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha kazi zote zinazotekelezwa zinakamilishwa ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa

“Serikali imetumia fedha nyingi sana kuwekeza katika SGR, ni wajibu wetu kuhakikisha miundombinu hii tunaitunza, tunailinda na kuendelea kuiimarisha kwa nguvu kubwa kwani huu ni uwekezaji wa Taifa ambao lazima tuulinde,” amesisitiza Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa ameitaka TRC kuhakikisha huduma za SGR zinaendelea kupatikana kwa ufanisi na usalama wakati wote, iwe mvua au jua, kwa kuimarisha maandalizi na mifumo ya kukabiliana na changamoto za hali ya hewa kwa lengo la kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa wa Serikali unaleta huduma salama, endelevu na za uhakika kwa Watanzania

Kwa upande wake,  Kaimu Mkurugenzi wa miundombinu na ujenzi wa TRC Mha. Ismail Athuman ameelezea hatua zinazochukuliwa na Shirika katika kukabiliana na athari za mvua, ikiwemo ufuatiliaji wa maeneo hatarishi, ukaguzi wa miundombinu, maandalizi ya vifaa na wataalamu.