MANUNUZI BORA KUWA CHACHU YA UKAMILISHAJI WA MIRADI YA KIMKAKATI
Maafisa ugavi na manunuzi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi wametakiwa kuimarisha ufanisi katika shughuli za manunuzi ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa ubora unaokusudiwa na kuzingatia thamani halisi ya fedha za umma zinazowekezwa
Akifungua kikao kazi cha saba cha Wakuu wa Vitengo vya Menejimenti ya Ununuzi na Ugavi vilivyopo chini ya Wizara ya Uchukuzi tarehe 23 Nov, 2026 Mkoani Kigoma kwa niaba ya katibu mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Godius Kahyarara, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Lucas Kambelenje, amesema manunuzi yanapaswa kuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini
Amesema Maafisa manunuzi hawapaswi kujikita katika kuzingatia matakwa ya sheria pekee, bali kuhakikisha bidhaa na huduma zinazopatikana zinakidhi viwango vya ubora na kuchangia ukamilishaji wa miradi kwa wakati na kwa thamani stahiki ya fedha na kusisitiza umuhimu wa nidhamu katika matumizi ya fedha, ununuzi na usimamizi wa mali za umma
Vilevile, amewataka wakuu wa vitengo vya manunuzi na ugavi kuimarisha ushirikiano na mahusiano baina ya taasisi ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi ya umma
Awali, Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Johnson Laizer, alisema kikao hicho cha siku tatu kinalenga kubadilishana uzoefu na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji bora katika ununuzi, usimamizi wa mikataba na mali za umma
Ameongeza kuwa kikao hicho kitatoa fursa ya kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili watendaji hao katika kusimamia miradi ya kimkakati ya kitaifa, pamoja na kubainisha hatua za kuboresha utendaji na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma.
