BILIONI 434 KUKAMILISHA UJENZI WA BANDARI YA KISIWA MGAO
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 434 katika ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara na itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi
Prof. Mbarawa ameyasema hayo Novemba 22, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo, akieleza kuwa Serikali imehakikisha upatikanaji wa fedha za mradi na hivyo kuondoa changamoto zilizokuwa zikikwamisha utekelezaji wake na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuzingatia ratiba iliyowekwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa
Amesema bandari hiyo itakuwa na gati lenye urefu wa mita 500 na upana wa mita 40, hatua itakayosaidia kutatua changamoto ya kuchanganya mizigo ya kawaida na mizigo maalumu ikiwemo makaa ya mawe, saruji na mbolea katika Bandari ya Mtwara. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati miundombinu saidizi ikiwemo barabara na mfumo wa kusafirisha mizigo kwa mikanda (Conveyor Belt) ili viende sambamba
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameipongeza Serikali kwa kuhakikisha changamoto zilizokuwa zikikwamisha mradi zinapatiwa ufumbuzi, huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia asilimia 85 ya maendeleo ya ujenzi ifikapo Machi 2027 na kusisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kufanya ziara za ukaguzi wa mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya mradi huo
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Erick Kadinda, amesema mradi huo umefikia asilimia 57 ya utekelezaji na pindi utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia tani milioni moja za mizigo kwa mwaka, pamoja na kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 200,000 za makaa ya mawe na kuongeza kuwa kwa sasa hakuna changamoto za kifedha na kazi zinaendelea
Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Mbunge wa Newala Mjini, Mhe. Rashid Mtima, amesema bandari hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa Mtwara na kuifanya kuwa kitovu cha uchumi wa kusini.
