Usafiri Majini kufanyiwa Maboresho Makubwa – Serikali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalam wa wizara hiyo pamoja na timu ya Mshauri Elekezi atakayefanya utafiti wa awali ikiwa ni hatua ya kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Usafiri Majini.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki yalilenga kujadili hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya utafiti huo muhimu kwa sekta ya usafiri wa majini nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Kahyarara amesema kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa wa kisasa, salama na wenye tija kwa uchumi wa taifa, hususan katika maeneo yenye fursa kubwa za biashara na utalii kama vile Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa pamoja na ukanda wa Bahari ya Hindi.
“Sera hii mahsusi ya usafiri majini itakuwa nyenzo muhimu ya kutatua changamoto za kisera katika kuhakikisha miundombinu ya usafiri majini inaboreshwa, usalama wa abiria na mizigo unaimarishwa, na sekta hii inachangia kikamilifu pato la taifa,” amesema Prof. Kahyarara.Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Mshauri Elekezi, Kapteni Ibrahim Bendera, aliihakikishia Serikali kuwa tayari Timu yake imeanza taratibu za awali za kazi hiyo, ikiwemo kukusanya nyaraka muhimu, kuanisha wadau wakuu na kuainisha nchi ambazo zimepiga hatua kubwa kwa ajili ya kupata uzoefu katika sera zao hususan nini kilifanyika kwa ujumla kutatua changomoto. Nchi zilizotajwa kufanyiwa mapitio ni pamoja na Singapore na ufilipino.
Utafiti huo unatarajiwa kuchukua miezi mitatu na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2025.