Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

USAFIRI KWA NJIA YA MAJI KIPAUMBELE SEKTA YA UCHUKUZI

Imewekwa: 20 Nov, 2023
USAFIRI KWA NJIA YA MAJI KIPAUMBELE SEKTA YA UCHUKUZI

Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika usafiri kwa njia maji hususani katika Maziwa yaliyopo nchini ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo baina ya mikoa na nchi jirani zinazozunguka maziwa hayo.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa meli ya MV. Umoja na utiaji saini mikataba mitatu ya ukarabati wa meli Mkoani Mwanza Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amesema utiaji saini huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuwaletea maendeleo wananchi kupitia usafiri wa maji.

 

“Mwezi mmoja uliopita Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli ilisaini mikataba mitatu ya ujenzi na ukarabati wa Meli ziwa Tanganyika leo tunazindua meli na kusaini mikataba mingine ya ukarabati wa meli nyingine, miradi hii inaonyesha kwa vitendo dhamira ya Serikali kwa wananchi wake” amesema Naibu Waziri Kihenzile.

 

Naibu Waziri Kihenzile amesema kukamilika kwa uwekezaji wa miradi ya ukarabati na ujenzi wa meli kunatarajiwa kuongeza pato la nchi, mikoa na wananchi kwa ujumla kwani kutaruhusu usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka eneo moja kwenda jingine kwa wakati na kuwezesha kushuka kwa bei za bidhaa.

 

Aidha, Naibu Waziri kihenzile ameeleza umuhimu wa utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo upatikanaji wa ajira kwa wananchi wanaokaa katika maeneo inapotekelezwa na kutumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi watakaopata kazi kutojihusisha na vitendo vya uhujumu ili mradi ukamilike kwa wakati na viwango.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amina Makilagi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini kwa kujenga na kukarabati meli kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza uchumi wa mikoa inayozunguka kanda ya Ziwa Viktoria.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Meja Jenerali (Mstaafu) John Mbungo amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa bodi imejipanga kusimamia miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaokane wakati wa utekelezaji na baada ya kukamilika.

 

Serikali kupitia MSCL imesaini mikataba mitatu ukiwemo wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba iliyopo mkoani Kigoma utakaofanywa kwa ushirikiano wa kampuni ya M/S Brodosplit JSC ya Nchini Croatia na Kampuni ya M/S Dar es Salaam Merchant Group kwa gharama ya shilingi bilioni 32, Ukarabati wa MT. Ukerewe utakaofanywa na Kampuni ya  M/S Dar es Salaam Merchant Group kwa gharama ya shilingi bilioni 6 na ukarabati wa meli ya MT. Nyangumi utakaofanywa na Kampuni ya M/S Dar es Salaam Merchant Group kwa gharama ya shilingi bilioni 8.