TPA YATAKIWA KUENDELEA KUTAFUTA WATEJA WA KUTUMIA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Mwenyekiti wa kamati ya Miundombinu Selemani Kakoso (MB) ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuendelea kutafuta wateja katika nchi za Uganda , DRC Kongo na Sudani ya Kusini.
Kakoso ameyasema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Miundombinu ya kujadilia taarifa za utendaji kazi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jijini Dodoma.
“ Bandari Dar es Salaam inauwezo wa kuhudumia mizigo kutoka DRC -Kongo, Uganda , Zambia na Malawi kwa kiwango kikubwa hivyo TPA hakikisheni mnakwenda kutafuta wateja katika nnchi hizo”, Alisema Kakoso.
Pia Kamati hiyo ya miundombinu imeagiza TPA kuhakikisha wanakamilisha Mchakato wa Ujenzi wa Matanki ya Mafuta katika eneo la kigamboni kwani matanki hayo ya mafuta yatakuwa na uwezo wa kupokea mafuta kiasi cha mita za ujazo 360,000. Ambapo ujenzi wake upo katika hatua za manunuzi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihanzile amesema kuwa Wizara ya Uchukuzi na TPA wanaendelea na kazi ya Kuandaa mpango kabambe wa kufikia masoko ya nchi za Uganda, Malawi, DRC-Kongo, Zambia , na Zimbambwe.
Kihanzile amesema kuwa Serikali inandelea na mchakato wa kujenga kuboresha miundombinu ya usafishaji katika ukanda wa kusini mpaka ziwa Nyasa, pamoja na uboreshaji wa Barabara na Reli katika Bandari ya Kalema na kuboresha ujenzi wa Meli katika ziwa Tanganyika na Victoria.
Huku naibu mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Juma Kijava amesema kuwa kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea na uboreshaji wa Bandari ya Tanga, Kigoma, Mtwara na Nyingine.