Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

TAZARA YAPONGEZWA KWA KASI YA UREJESHAJI MIUNDOMBINU ILIYOHARIBIWA

Imewekwa: 29 May, 2024
TAZARA YAPONGEZWA KWA KASI YA UREJESHAJI MIUNDOMBINU ILIYOHARIBIWA

 

 

Mamlaka ya reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA) imepongezwa kwa kasi kubwa ya urejeshaji wa miundombinu ya reli iliyoharibiwa

 

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe. David Kihenzile wakati wa  ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za urejeshwaji wa miundombinu na  huduma za usafiri wa treni ya Tazara kwa kipande cha Ifakara mpaka Lumumwe ambazo zilisimama kupisha urekebishaji wa miundombinu iliyoharibiwa kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha Nchini.

 

"Nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya wakati ule nilikuja kwa helkopta miundombinu haikuruhusu kufika hapa ila safari hii nimekuja na kiberenge nimejionea tayari panafikika na kazi kubwa imeshafanyika na changamoto zote mlizosema nimezichukua" amesema kihenzile

 

Ameongeza kuwa lengo la ziara hii ni kujionea tangu alipofika mara ya mwisho tarehe 4 mwezi Mei, maendeleo yaliyofikiwa na kipi kinatakiwa kuongezewa nguvu ili kuhakikisha usafiri wetu kwenye reli hii ya kihistoria ya Tazara unarejea kama ilivyokuwa mwanzoni kutoka Dar es salaam mpaka Kapiri Mposhi,Zambia

 

"Pamoja na kufurahia kazi nzuri iliyofanyika hapa na nimeona treni za mizigo zimeanza kupita hapa natoa maelekezo tena Tazara simamieni maeneo yote yaliyobakia ili kuhakikisha reli yote inarudi katika hali yake huku tukizingatia usalama wa abiria na mizigo ili usafirishaji wa abiria uanze mara moja" amesisitiza Kihenzile

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya amemshukuru Naibu Waziri wa Uchukuzi kwa usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maendeleo ya urejeshwaji wa miundombinu ya Reli ya Tazara kwenye wilaya ya Kilombero na kusisitiza kuwa kama wilaya wataendelea kutoa ushirikiano kila watakapohitajika ili kuhakikisha miumdombinu inakamilika kwa wakati na huduma zinarejea kwa wananchi

 

Akizungumzia maendeleo ya urejeshaji wa miundombinu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tazara Mha. Kelvin Kyara ameishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kutoa fedha na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ukarabati huo ambao uko mwishoni kukamilika kabisa ili kurejesha huduma zilizokuwa zimesimama kwa zaidi ya mwezi mmoja