Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

TANZANIA YAZIDI KUJENGA HADHI YAKE KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI, YAPEWA UENYEKITI MWENZA JUKWAA LA MAWAZIRI BEIJING

Imewekwa: 22 Sep, 2026
TANZANIA YAZIDI KUJENGA HADHI YAKE KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI, YAPEWA UENYEKITI MWENZA JUKWAA LA MAWAZIRI BEIJING

Tanzania imepewa nafasi ya Uwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi linalofanyika jijini Beijing, China ambapo Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameshiriki katika jukwaa hilo leo tarehe 22 Septemba 2026, akiongoza kwa pamoja na Waziri wa Uchukuzi wa China, Mhe. LIU Wei

Jukwaa hilo la siku tatu limewakutanisha zaidi ya Mawaziri 20 wa Uchukuzi kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujadili maendeleo ya sekta hiyo, kubadilishana uzoefu na kuimarisha miundombinu na huduma za usafirishaji, pia linahamasisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa China wa Global Development Initiative (GDI)

Akizungumza katika jukwaa hilo, Prof. Mbarawa amesema Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika reli ya kisasa, barabara, bandari na viwanja vya ndege,amesema uwekezaji huo unalenga kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo, kuunganisha maeneo ya vijijini na mijini, kuchochea biashara na kuongeza fursa za kiuchumi

Aidha, Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kuwaalika taasisi za serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza Tanzania, akisisitiza kuwa Sekta ya Uchukuzi ina fursa mbalimbali za uwekezaji “Tanzania ina fursa nyingi kupitia Sekta ya Uchukuzi, hivyo ninawaalika taasisi za serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya Uchukuzi Tanzania,” amesema

Ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo unaipa fursa ya kushirikisha uzoefu wake, kujifunza teknolojia na mbinu kutoka nchi nyingine, pamoja na kutafuta fursa za uwekezaji katika miradi ya uchukuzi

Tanzania na China zina historia ya muda mrefu ya ushirikiano katika Sekta ya Uchukuzi, ikiwemo reli ya TAZARA na usafiri wa majini kupitia SINOTASHIP, Nafasi ya Uwenyekiti Mwenza inaongeza fursa za kuendeleza ushirikiano huo katika miundombinu, teknolojia na uwekezaji.