NAIBU WAZIRI AMWAKILISHA WAZIRI MKUTANO WA ACOSCM
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amemwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa kufungua Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026), unaofanyika Arusha Septemba 22 na 23, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Waziri Kihenzile amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya uchukuzi kwa lengo la kuunganisha reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege na kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. Hawa Tundu, amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa wataalamu na wadau kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuboresha mifumo ya mnyororo wa ugavi barani Afrika.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kühne Foundation Tanzania, Dkt. Beatrice Millu, amesema ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu na sekta binafsi ni muhimu katika kujenga wataalamu wenye uwezo na kuimarisha sekta ya usafirishaji na ugavi.
Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha zaidi ya washiriki 200 kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili mikakati ya kujenga mifumo ya ugavi yenye ustahimilivu, ubunifu na uendelevu kwa maendeleo ya Afrika.
