TANZANIA YATAKA USHIRIKIANO IMARA KUIMARISHA USALAMA WA BAHARINI AFRIKA
Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kuimarisha maandalizi ya usalama wa baharini, utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na ushirikiano wa kikanda ili kukabiliana na vitisho vinavyojitokeza katika maeneo ya bahari.
Wito huo umetolewa Novemba 19, 2026, na Mkurugenzi wa Uchukuzi, Mazingira na Usalama wa Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo, wakati wa majadiliano ya jopo katika Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Taasisi za Usimamizi wa Masuala ya Bahari Afrika (AAMA), uliofanyika Kampala, Uganda.
Bi. Katondo amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali, kuweka wazi majukumu ya kila taasisi na kuhakikisha maamuzi yanayokubaliwa yanatekelezwa kwa ufanisi. Pia ameitaka AAMA kuimarisha uratibu kati ya Mkataba wa Djibouti na Mfumo wa Yaoundé katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama baharini.
Amesema usalama wa baharini unapaswa kupewa kipaumbele kiuchumi na kisiasa kutokana na mchango wake katika kulinda biashara ya kimataifa, uvuvi, uwekezaji, maisha ya jamii za pwani na usalama wa mabaharia.
