Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 10 WA MAWAZIRI WA UCHUKUZI WA MOESNA

Imewekwa: 13 Oct, 2026
TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 10 WA MAWAZIRI WA UCHUKUZI WA MOESNA

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Baraza la Mawaziri la Kanda ya Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOESNA), utakaofanyika Oktoba 15, 2026, kwenye Hoteli ya Johari Rotana,Jijini Dar es Salaam,  Mkutano ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri 26 wanaosimamia sekta ya uchukuzi na lojistiki kutoka nchi wanachama

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026, Kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema mkutano huo utajadili mikakati ya kuimarisha uunganishaji wa nchi wanachama, kurahisisha biashara na kukuza ushirikiano katika sekta ya uchukuzi

Amesema ajenda muhimu ni kupanua usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya maji kati ya bandari za Afrika, pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayoongeza ushindani wa bara hilo katika usafirishaji kwa njia ya maji na masoko ya kimataifa. Aidha, MOESNA inalenga kuhamasisha uanzishwaji wa mashirika ya meli barani Afrika yatakayoweza kushindana katika soko la kimataifa.

Kihenzile amesema MOESNA pia imeamua kuanzisha chuo kikuu cha kikanda kitakachojikita katika elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu wa usafiri wa majini, kitakachojengwa nchini Tanzania na kueleza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na MOESNA pamoja na nchi wanachama kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya kikanda

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa MOESNA, Bw. Kassim Mpaata, amesema maandalizi ya ujenzi wa chuo hicho yameendelea kupata ushirikiano kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo Tanzania na Botswana na kuongeza kuwa Mkutano huo utashirikisha wawakilishi wa Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), AfCFTA na jumuiya za kiuchumi za kikanda

Usafirishaji wa majini ni sehemu muhimu ya biashara ya kimataifa ya Afrika, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya bara hilo husafirishwa kwa njia ya maji. Mkutano huo unatarajiwa kutoa fursa ya kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika biashara na maendeleo ya kiuchumi.