TANZANIA KURUHUSU WATOA HUDUMA WENGINE KATIKA RELI ZAKE
Serikali imesema mabadiliko ya Sheria ya Reli Nchini yatakayoruhusu watoa huduma wengine kutumia reli za Tanzania yataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usafirishaji na hivyo kuinua pato la nchini.
Akizungumza katika kikao cha Ushoroba wa Kati kilichohudhuriwa na Makatibu Wakuu wa Uchukuzi kutoka Rwanda, Uganda, Burundi, Malawi, Zambia, Tanzania na DRC, kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara amesema sekta ya usafirishaji ikiimarishwa itarahisisha mwenendo wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na hivyo kuwafikia walaji kwa wakati.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan imejikita kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakuwa na kuchangia zaidi pato la Taifa ndio maana kumekuwa na jitihada za makusudi za maboresho katika sekta ndogo hiyo ikiwemo kwenye miundombinu na sheria zinazosimamia usafiri huo”. amesema Prof. Kahyarara.
Katibu Mkuu Prof. Kahyarara amesema dhamira ya Serikali inaonyeshwa kwa vitendo kwani tayari mradi wa ukarabati wa meli MV. Umoja inayobeba mabehewa takribani 22 imeshakamilika na itaanza kufanya kazi mapema mwezi oktoba kutoka Bandari ya Mwanza kuelekea Port Bell Uganda.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi toka Burundi Chrisine Niragira amesema nchi wanachama wa Ushoroba wa Kati wakijiimarisha kwenye reli kutatoa nafasi kwa mzigo mkubwa zaidi kusafirishwa kwa wakati mmoja na hivyo kunusuru uharibifu wa miundombinu mingine kama barabara.
Kupitia kikao hicho cha siku moja wananchama hao wameongeza wananchama kwa kuziongeza nchi za Malawi na Zambia na hivyo kufanya Ushoroba wa Kati kuwa na wanachama saba.