Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

TALTA YAZINDULIWA RASMI

Imewekwa: 16 May, 2025
TALTA YAZINDULIWA RASMI

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe David Kihenzile kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezindua rasmi Chama cha Wataalam wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA) akisisitiza kuwa chama hicho ni mhimili muhimu katika kuimarisha weledi na utoaji wa huduma bora katika sekta ya uchukuzi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu Cha Dar es salaam tarehe 09 Mei,2025 Kihenzile amesema TALTA inawakilisha wataalam wenye elimu na uzoefu wa ngazi mbalimbali na itakuwa kichocheo katika kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Wataalam wa Uchukuzi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya uchukuzi kupitia reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na vyuo vya mafunzo ili kukuza usafirishaji nchini

Ametoa rai kwa wataalam wote kujiunga na TALTA, Taaasisi za Serikali na binafsi kuwapa fursa wataalam wao kujiunga, na uongozi wa TALTA kuhakikisha chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata katiba, weledi na kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.

Akitoa Salam za Wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof Godius Kahyarara, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Usafiri Bw. Andrew Magombana ameahidi ushirikiano wa karibu na TALTA katika kutekeleza Sera,Mikakati na maboresho ya huduma za uchukuzi kwa lengo la kuhakikisha usalama,ufanisi na haki kwa watumiaji wote

Kwa upande wake rais wa TALTA  Bw. Alphonce Mwingira ameeleza dhamira ya chama ni kuwaunganisha wataalam kwa njia mbalimbali na kushirikiana na Serikali na sekta binafsi katika kukuza taaluma ya lojistiki na usafirishaji huku akisisitiza kigezo cha kuwa mwanachama ni kuwa na elimu ya ngazi yoyote ya lojistiki na usafirishaji kutoka chuo kinachotambulika na Serikali.