Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SHILINGI BILIONI 379 KUIMARISHA UZALISHAJI WA MATALUMA YA RELI NCHINI

Imewekwa: 26 Oct, 2026
SHILINGI BILIONI 379 KUIMARISHA UZALISHAJI WA MATALUMA YA RELI NCHINI

Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 379 katika Kiwanda cha Mataluma ya Reli cha Uyumbu, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa kuagiza mataluma kutoka nje ya nchi.

Akizungumza mkoani Tabora, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi na kuhakikisha upatikanaji wa mataluma yenye ubora kwa ajili ya reli za kisasa (SGR) na za zamani (MGR).

Waziri Prof. Mbarawa amesema uzalishaji wa mataluma nchini utasaidia kupunguza gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya reli, huku ukiongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo.

Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kiwanda hicho ili kuhakikisha kinafikia malengo ya uzalishaji na kukidhi mahitaji ya sekta ya reli nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Shiwa, amesema kiwanda hicho kitachangia kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa treni za SGR na MGR.

Mhandisi Machibya ameongeza kuwa kiwanda hicho kina fursa ya kukuza biashara kwa kuuza mataluma katika nchi nyingine, kuongeza mapato na kuimarisha sekta ya viwanda pamoja na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.