MITAWI AONGEZA MSUKUMO WA KUBORESHA HUDUMA ZA UCHUKUZI NA USALAMA WA ANGA MWANZA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. Abdallah Mitawi, leo tarehe 26 Oktoba, 2026 amefanya ziara ya kikazi katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kukagua utekelezaji wa majukumu ya taasisi za uchukuzi, kutathmini ubora wa huduma na kuhimiza uboreshaji wa usalama na ufanisi wa usafiri wa anga
Katika ziara hiyo, alipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu utekelezaji wa majukumu yao, huduma zinazotolewa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa pamoja
Akizungumza baada ya kutembelea miradi, Mhe Mitawi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi hizo, akieleza kuwa sekta ya uchukuzi, hususan usafiri wa anga, ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi, utalii na upatikanaji wa fedha za kigeni na kubainisha kuwa mchango huo unaendana na mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
Aidha, amesisitiza ukaguzi wa mara kwa mara wa mipaka ya viwanja vya ndege ili kuzuia uvamizi wa maeneo na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi na kuzitaka taasisi husika kuimarisha tahadhari za hali ya hewa na maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El nino ili kulinda miundombinu na usalama wa safari za ndege
Awali Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza Bw. Stevius Mfuko alieleza hatua zinazochukuliwa kuboresha uendeshaji na huduma kwa abiria na mashirika ya ndege na namna ya uendeshaji huku wawakilishi wa ATCL, TCAA na TMA nao wakiwasilisha taarifa kuhusu usalama wa anga, ufanisi wa safari na upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wakati
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Uchukuzi za kufuatilia utendaji wa taasisi, kubaini changamoto na kuimarisha utoaji wa huduma bora na salama, huku sekta ya anga ikiendelea kuchangia maendeleo ya uchumi, utalii na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
