Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SERIKALI YAZITAKA TAASISI KUIMARISHA USALAMA WA ANGA

Imewekwa: 30 Nov, 2025
SERIKALI YAZITAKA TAASISI KUIMARISHA USALAMA WA ANGA

Serikali imezitaka taasisi zote zinazofanya kazi katika Viwanja vya ndege Nchini  kutekeleza kikamilifu mafunzo, maarifa na maelekezo yaliyotolewa katika wiki ya mafunzo ya usalama wa anga ili kuongeza ufanisi wa shughuli za viwanja vya ndege na kuvutia mashirika zaidi ya ndege kufanya safari nchini.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Maadhimisho ya Utamaduni wa Usalama wa Usafiri wa Anga yaliyofanyika katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile, amesema ongezeko la mashirika ya ndege yatakayotoa huduma za usafiri wa ndani na nje litaiwezesha Tanzania kuunganishwa zaidi na mataifa mbalimbali duniani na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi itaendelea kutenga fedha za ujenzi , ukarabati na ununuzi wa vitendea kazi na kuendeleza rasilimali watu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwenye viwanja vya ndege nchini zinakidhi viwango vya kimataifa sambamba na kuongeza uaminifu kwa watumiaji na wadau wa sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Bi. Irene Minja, ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, alisema TAA imejipanga kuhakikisha viwanja vyote nchini vinaendelea kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya washitiri na kuongeza ufanisi wa huduma.

Amesema mafanikio yanayoonekana katika viwanja vya ndege nchini ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zote zinazofanya kazi katika mazingira ya viwanja vya ndege, hatua inayochochea utendaji bora na kuongeza ubora wa huduma.