Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SERIKALI YATOA MSUKUMO WA SAYANSI, TAFITI NA TEKNOLOJIA KUKUZA UCHUMI WA BULUU

Imewekwa: 08 Sep, 2026
SERIKALI YATOA MSUKUMO WA SAYANSI, TAFITI NA TEKNOLOJIA KUKUZA UCHUMI WA BULUU

Serikali imesisitiza kuimarisha sayansi, tafiti, ubunifu na teknolojia ili kukuza Uchumi wa Buluu na kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na bahari, maziwa, mito na maeneo ya pwani kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yamesemwa leo, Septemba 7, 2026, jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Masauni, kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akifungua Kongamano la Tano la Kimataifa la Sayansi na Uchumi wa Buluu (IBEC 2026), lililoandaliwa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), linalofanyika hadi Septemba 9, 2026, likiwa na kaulimbiu “Kuwezesha Shughuli za Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo Endelevu.”

Masauni amesema tafiti zinapaswa kulenga kutatua changamoto za sekta, kuongeza thamani ya rasilimali za majini, kuboresha uzalishaji na kuhifadhi mazingira na kuongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeutambua Uchumi wa Buluu kuwa eneo la kimkakati katika kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu

Akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika rasilimali watu, teknolojia, elimu, utafiti na ubunifu ili Tanzania inufaike na fursa za Uchumi wa Buluu, huku DMI ikiwa na nafasi muhimu ya kuunganisha elimu, tafiti na mahitaji ya kisekta

Kihenzile amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na mifumo ya usafiri ili kuongeza biashara, uwekezaji na ushindani wa Tanzania, huku akihimiza sekta binafsi kutumia fursa za teknolojia za baharini, kuongeza thamani ya mazao ya bahari, biashara ya kaboni buluu na huduma za kidijitali

Awali, Mkuu wa  Chuo cha DMI, Prof. Tumaini Gurumo, amesema IBEC 2026 ni jukwaa muhimu la kuunganisha watafiti, watunga sera, sekta binafsi, taasisi za elimu na wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania katika kujadili fursa za uwekezaji, ajira, teknolojia, rasilimali watu na uhifadhi wa mazingira katika Uchumi wa Buluu.