Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MITAWI AITAKA DMI KUANDAA WATAALAMU WENYE UJUZI NA WELEDI KUKABILI MAHITAJI YA SEKTA YA UCHUKUZI

Imewekwa: 01 Sep, 2026
MITAWI AITAKA DMI KUANDAA WATAALAMU WENYE UJUZI NA WELEDI KUKABILI MAHITAJI YA SEKTA YA UCHUKUZI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, ametembelea Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), ambapo amesisitiza umuhimu wa Chuo hicho kuendelea kuandaa wataalamu wenye ujuzi, weledi na uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya uchukuzi nchini

Katika ziara hiyo, Bw. Mitawi amefanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo, Prof. Tumaini Gurumo, na kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Chuo, hususan katika utoaji wa elimu na mafunzo yanayolenga kuzalisha wataalamu katika kada mbalimbali za sekta ya uchukuzi

Naibu Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa DMI kuendelea kuboresha programu za mafunzo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira na viwango vya kimataifa, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta

Aidha, ameitaka DMI kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya uchukuzi ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwekeza katika tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, hatua zitakazosaidia kuongeza ubora wa mafunzo na ushindani wa wataalamu wa Tanzania

Awali Mkuu wa Chuo Cha Bahari Dar es salaam(DMI) Prof. Tumaini Gurumo, alieleza kuwa DMI ina jukumu la msingi la kutoa elimu, mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wanaohitajika katika sekta ya bahari na uchukuzi kwa ujumla

Prof. Gurumo amesema Chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuimarisha programu za mafunzo na kutumia teknolojia za kisasa ili kukidhi mahitaji ya sekta na soko la ajira.