Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

NIT YATAKIWA KUIMARISHA MAFUNZO NA KUZALISHA WATAALAMU WENYE UJUZI UNAOKIDHI VIWANGO VYA KIMATAIFA

Imewekwa: 01 Sep, 2026
NIT YATAKIWA KUIMARISHA MAFUNZO NA KUZALISHA WATAALAMU WENYE UJUZI UNAOKIDHI VIWANGO VYA KIMATAIFA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, amekitaka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuendelea kuimarisha ubora wa mafunzo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na mabadiliko katika sekta ya uchukuzi, ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi na umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira kitaifa na kimataifa

Bw. Mitawi ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake kwenye chuo cha  NIT, ambapo alipokea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Chuo, programu zinazotolewa, miradi ya maendeleo na mikakati ya kuimarisha mafunzo kwa vitendo na kusisitiza umuhimu wa kuboresha mitaala na mazingira ya mafunzo ili kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya sekta ya uchukuzi

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu amekagua mitambo, vifaa na miundombinu ya mafunzo, akisisitiza kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa zitakazowawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta na kuongeza uwezo wao wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi

Aidha, Bw. Mitawi ameitaka NIT kuimarisha tafiti na ubunifu kwa kuelekeza tafiti katika kutafuta suluhu za changamoto halisi zinazoikabili sekta ya uchukuzi, ikiwemo kuboresha mifumo ya usafirishaji, kuongeza ufanisi na kuchochea matumizi ya teknolojia katika maendeleo ya sekta hiyo

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amemweleza Naibu Katibu Mkuu kuhusu programu na kozi zinazotolewa, miradi inayotekelezwa pamoja na jitihada za Chuo kuboresha mazingira ya mafunzo, akieleza kuwa NIT itaendelea kuimarisha mafunzo kwa vitendo, matumizi ya teknolojia, utafiti na ubunifu ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sekta ya uchukuzi na kuchangia maendeleo ya Taifa.