Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Serikali yashauriwa kuongeza ardhi mradi wa Bandari ya Kisiwa Mgao

Imewekwa: 10 Sep, 2026
Serikali yashauriwa kuongeza ardhi mradi wa Bandari ya Kisiwa Mgao

Serikali imeshauriwa kuongeza maeneo ya kutosha yanayozunguka Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara ili kuepusha gharama kubwa za fidia na ununuzi wa ardhi zitakazoweza kujitokeza wakati wa upanuzi wa bandari hiyo katika siku zijazo.

Ushauri huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, wakati Kamati hiyo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao.

Mwenyekiti Mheshimiwa Kakoso amesema uzoefu unaonyesha kuwa kuchukua maeneo madogo kwa ajili ya miradi mikubwa husababisha ongezeko la gharama pale inapohitajika kupanua maeneo hayo.

Mheshimiwa Kakoso pia amesisitiza umuhimu wa kuanza kwa wakati ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami itakayounganisha bandari hiyo na barabara kuu inayounganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara ili kuhakikisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inakamilika kwa pamoja na barabara na kuwezesha shughuli za bandari kuanza mara tu baada ya mradi kukamilika kwake.

Aidha, Kamati hiyo imeitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuendeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko katika maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za ujenzi, huku ikiutaka uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kusimamia haki za msingi za wafanyakazi, ikiwemo usalama kazini, bima za afya na matumizi sahihi ya fedha za ushuru wa Huduma na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali itafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kuendelea kusimamia Miradi ya Sekta inayotekelezwa mkoani Mtwara ili ikamilike kwa wakati na Viwango.

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Dkt. Baraka Mdima amesema mradi wa Ujenzi wa  Bandari ya Kisiwa Mgao unatekelezaa kwa Sh bilioni 435 na unajengwa mahsusi kuhudumia mizigo michafu iliyokuwa ikipitia Bandari ya Mtwara na kusababisha athari za kimazingira na ameongeza kuwa kwa sasa umefikia asiliamia  48 na  unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka 2028.