Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Serikali yapongeza Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Sumbawanga

Imewekwa: 24 Feb, 2026
Serikali yapongeza Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Sumbawanga

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameipongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kusimamia kwa ufanisi ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga uliogharimu takribani Sh bilioni 60.

Akizungumza mkoani Rukwa wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Naibu Waziri Kihenzile amesema hatua iliyofikiwa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji, huku akibainisha kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linatarajiwa kuanza safari zake katika kiwanja hicho kuanzia Machi 2026 mara baada ya taratibu za kuanza safari hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile, aliishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo na kusema kuwa utekelezaji huo umejibu kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Mkoa wa Rukwa waliokuwa wakitegemea zaidi usafiri wa barabara peke yake.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Mha. Joseph Gimonge  amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaufungua zaidi mkoa huo kwa kuchochea sekta ya utalii na biashara,utalii kupitia   Hifadhi ya Taifa ya Katavi na Maporomoko ya Kalambo na Ziwa Tanganyika, ambavyo ni miongoni mwa maeneo yenye mvuto mkubwa kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 96, umehusisha ujenzi wa barabara ya kurukia na kutua ndege yenye urefu wa mita 1,750 na upana wa mita 30 kwa kiwango cha lami, barabara za viungio (taxiways), maegesho ya ndege (apron), pamoja na jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 150,000 kwa mwaka. Pia umejumuisha ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege, barabara ya kuingia uwanjani, kituo kidogo cha umeme, uzio wa usalama na jengo la hali ya hewa.