Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Serikali yaongeza kasi ujenzi viwanja vya ndege

Imewekwa: 22 Dec, 2025
Serikali yaongeza kasi ujenzi viwanja vya ndege

Serikali imeongeza kasi ya uwekezaji katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini, ikisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usafiri wa anga na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Akizungumza mkoani Morogoro leo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Mwakiposa Kihenzile, amesema kukailika kwa miradi inayotekelezwa katika viwanja mbalimbali imeanza kuzaa matunda, ikiwemo kuongezeka kwa mashirika ya ndege yanayotoa huduma nchini na idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga.

Alisema uboreshaji wa miundombinu hiyo umechochea ukuaji wa sekta za utalii na biashara pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, huku akisisitiza kuwa jukumu la watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ni kuitunza na kuilinda miundombinu hiyo.

Naibu Waziri huyo aliwataka watumishi wa TAA kuimarisha uwajibikaji na mshikamano kazini, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia miradi kwa kuzingatia thamani ya fedha ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, amesema mamlaka inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wanaotoa huduma viwanjani ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya kimataifa, huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuitengea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.