Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SERIKALI YAIPA KIPAUMBELE SEKTA YA USAFIRI MAJINI :KIHENZILE

Imewekwa: 28 Sep, 2026
SERIKALI YAIPA KIPAUMBELE SEKTA YA USAFIRI MAJINI :KIHENZILE

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri majini ili kuongeza usalama, ufanisi, ushindani na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri Kihenzile ameyasema hayo Septemba 24, 2026, jijini Tanga wakati akifunga Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani 2026, yenye kaulimbiu “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora Katika Sekta ya Usafiri Majini.”

Amesema Tanzania ina nafasi muhimu katika usafiri majini kutokana na mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, huku Serikali ikiendelea kuboresha bandari, usalama wa vyombo, huduma za mizigo na abiria pamoja na matumizi ya teknolojia.

Aidha, amewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo kuhakikisha vinakidhi viwango vya usalama, vinafanyiwa ukaguzi na kuwa na leseni pamoja na vifaa vya kuokoa maisha. Pia amezitaka Wizara, TASAC na ZMA kujiandaa kukabiliana na athari za mvua kubwa za msimu wa Vuli 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amewataka wadau kutafsiri sera, sheria, viwango na mikataba ya kimataifa kwa vitendo ili kuimarisha usalama na ubora wa huduma.

Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema hadi Machi 2026, TASAC ilitoa vyeti 15,948 vya mabaharia, kutoka 10,270 mwaka 2024/25 na kuongeza kuwa Tanzania imekamilisha Kituo cha Kikanda cha Utafutaji na Uokoaji Mwanza na inaendelea na ununuzi wa boti za utafutaji na uokoaji.

Aidha, Mkurugenzi  Salum amesema TASAC  imeendelea na kampeni ya uhamasishaji kuhusu El Niño iliyofikia zaidi ya mikoa minane, bandari sita na vivuko vitatu.