Serikali yaahidi Mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara Uchukuzi

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inadhamira ya dhati ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji katika Sekta Uchukuzi.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, leo tarehe 19 Februari,2025 Jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Miaka 35 ya utoaji huduma ya Uchukuzi kwa Kampuni ya Superdoll hapa nchini.
Mhe. Prof. Mbarawa amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuwezesha sera na mifumo inayochochea ukuaji wa sekta ya Viwanda, maendelea ya miundombinu na kurahisisha ufanyaji biashara nchini.
Amesema Serikali ya Tanzania inatambua jukumu kubwa la miundombinu ya usafiri katika Maendeleo ya Taifa na hivyo inaendelea kupanua na kuufanya mtandao wa barabara kuwa wa kisasa zaidi, kuhakikisha mawasiliano kati ya maeneo ya mijini na vijijini yanaimarishwa na kuwezesha biashara ya mipakani na nchi jirani.
Pia, Waziri Mbarawa amesema maono ya Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na uchukuzi Afrika Mashariki, kati na kusini kwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara, reli na bandari inakuwa ya kiwango cha kimataifa na hivyo kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mpango huu utaongeza kiwango cha Shehena kinachopita kupitia bandari za Tanzania na kutengeneza fursa kubwa zaidi kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara kupitia Sekta ya Uchukuzi na hatimaye kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji na ustawi wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll Bw. Seif A. Seif ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara Nchini, na ndio kiini cha mafanikio yao ya kufanya biashara na kukuza Uwekezaji wao kwa miaka 35 sasa.
Maadhimisho haya yamehudhuriwa na Mabalozi wa Nchi za Ujerumani na Oman hapa nchini Mhe. Thomas Terstegen na Mhe. Saud Bin Hilal Al-Shaidhani, Mkurenzi Mkuu wa Latra CPA. Habibu Suluo, Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya BPW ya Ujerumani Bw. Tobias Wiedeking na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Fedha na Taasisi za Elimu ya Juu hapa nchini.