Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza Viwanja vya Ndege Nchini.

Imewekwa: 23 Feb, 2025
Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza Viwanja vya Ndege Nchini.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuingilia kati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kumekuwa sababu ya kuanza kutekelezwa kwa mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga.

Waziri Mbarawa ameyasema hayo jana alipotembelea uwanja huo kwa lengo la kuangalia maendeleo ya mradi wa ujenzi ulioanza mwanzoni mwa mwaka 2023.

"Mradi huu ulisainiwa mwaka 2017 tulipambana mradi uanze lakini kwa sababu mbalimbali ulishindikana, Niliporudi kwenye wizara mwaka 2022 Rais akanipa maelekeza mahsusi kuhakikisha mradi huu unaouhusisha viwanja vya Shinyanga, Katavi, Kigoma na Tabora unaanza," Alisema Mbarawa.

Prof. Mbarawa amewapongeza wakandarasi wa viwanja vyote vinne kwa kuvumilia tangu mwaka 2017 mkataba uliposainiwa licha ya kuchelewa kwa kiasi hicho lakini bado wamekuwepo isipokuwa mkandarasi mmoja wa kiwanja cha Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kukua kwa shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja usafirishaji wa madini yanayopatikana mkoani humo.

Kwa uapnde wake Mhandisi wa Mradi kutoka Tanroads ambao ndio waajiri katika mradi huo Donatus Binemungu amesema ujenzi wa mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 44.8 unahusisha ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, maingilio ya ndege (Taxiway), maegesho ya ndege (Apron) na jengo la abiria.

Binemungu amesema kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kupokea ndege za ukubwa wa aina ya Bombardier Q400 ambapo njia ya kutua na kurukia ndege ina urefu wa mita 2200.